Ajali za barabarani zinaua zaidi ya malaria kwa mwaka!
MATUKIO ya ajali za barabarani yamekuwa yakiwasababishia wananchi madhara makubwa yakiwemo kupoteza maisha, majeraha makubwa, ulemavu wa kudumu, mali kuharibika hata kupotea.
Ajali za barabarani zinazosababisha vifo na majeruhi wengi, zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kutokana na ajali hizo, mwaka 2007 watu 2,594 walifariki dunia, 16,308 walijeruhiwa. Vile vile mwaka 2008 watu 2,905 walifariki dunia, na majeruhi walikuwa 17,861.
Kutokana na hali hiyo wapatao 20,000 wengi wa waathirika wameachwa bila kujua hatma ya fidia zao baada ya kupatwa na madhara yaliyosababishwa na ajali za barabarani.
Ajali hizo zimekuwa zikichangia vifo vingi vya watoto na vijana duniani hasa walio na umri kati ya miaka 10 mpaka 24 na ni chanzo cha tatu kwa vifo vya watu walio na umri kati ya miaka 30 na 44.
Kutokana na ajali hizo kuongezeka ndio maana imetengwa siku maalum ya Kimataifa ya kuwakumbuka waathirika wa Ajali za Barabarani kila Mwaka Duniani.
Siku ya kuwakumbuka waathirika wa ajali za barabarani huadhimishwa kila ifikapo 15, Novemba ya kila mwaka.
Maadhimisho hayo yalianzishwa na Umoja wa Mataifa kwa kupitia katika Azimio lake la namba A/60/5(2005).
Siku hii inatambulika kama siku rasmi ya kimataifa ya kuwakumbuka waathirika wa ajali hizo za barabarani na familia zao na kuzitaka nchi wanachama pamoja na jumuiya za kimataifa kuitambua siku hiyo.
Hapa nchini siku hii ilianza kuazimishwa na Baraza la ushauri Watumaiaji wa Huduma za nchi Kavu na Majini (SUMATRA-CCC) Mwaka jana jijini Dar es Salaam.
Pia siku hiyo hutoa fursa kwa jamii nzima kukutana na kuwakumbuka wahanga wa ajali za barabarani kutafakari madhara, gharama, na hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kuzuia ajali zisitokee.
Siku ya kuwakumbuka wahanga wa ajali za barabarani inatoa nafasi ya kuikumbusha serikali wajibu wake na jamii nzima katika suala la kuzifanya barabara kuwa sehemu salama.
Kwa bara la Afrika siku hii imekuwa ikiadhimishwa maadhimisho katika nchi za Afrika ya Kusini, Uganda na Nigeria katika miaka iliyopita.
Takwimu zinaonyesha kuwa kila baada ya dakika 6, mtu mmoja hufa au kujeruhiwa kwa na ajali za barabarani duniani kote, wakiwemo madereva, abiria, waendesha pikipiki, baiskeli na watembea kwa miguu.
Takwimu za dunia zinaonesha kuwa watu milioni 1.2 hufa kutokana na ajali za barabarani kila mwaka na kuacha mamilioni ya watu na ulemavu wa kudumu duniani.
Idadi hii ya waathirika ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya watu wanaokufa kutokana na malaria.
Zaidi ya watoto 260,000 hufariki kila mwaka kutokana na ajali za barabarani duniani kote.
Shirika la Afya Duniani linaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2015, ajali za barabarani zitakuwa chanzo kikuu cha vifo na ulemavu kwa vijana.
Asilimia 90 ya vifo hivyo hutokea katika nchi zenye pato la kati na la chini, Tanzania ikiwa miongoni mwa kundi la pato la chini kabisa na kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwa kipindi cha kati ya mwezi Januari na Juni mwaka jana watu 1460 walifariki dunia na watu zaidi 8,373 walijeruhiwa kutokana na ajali za barabarani hapa nchini ambapo ilikuwa inaonyesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huo, kutakuwa na jumla ya vifo 3000.
Baraza la Sumatra-ccc linaiasa jamii itambue kuwa madhara yote haya ni mzigo mkubwa kwa nchi kama Tanzania.
Kwani kwa Mwaka 2006 tu ilikadiriwa kuwa ajali hizo zilileta hasara ya asilimia 3.4 ya pato la ndani la Taifa.
Hata hivyo Sumatracc inashauri kuwa iwapo kama jamii na serikali itakuwa makini, vifo hivi vinaweza kuepukika, kwani zaidi ya robo tatu ya vifo vyote husababishwa na makosa ya kibinadamu.
Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba madereva, waenda kwa miguu, waendesha baiskeli na watumiaji wengine wa barabara, hufanya makosa ambayo huishia kupoteza maisha yao au ya wengine.
Sumatra-ccc inaamini kwamba kwa kutoa elimu, uhandisi na usimamizi wa sheria za barabarani, kutasaidia kupunguza vifo visivyokuwa vya lazima.
Siku ya kuwakumbuka wahanga wa ajaali za barabara hutumika kuikutanisha jamii kwaajili ya kuwaombea marehemu waliofariki kutokana na ajali mbalimbali.
Mwenyekiti wa Baraza la Sumatra-ccc,Gilliard Ngewe anasema siku kama hiyo kila mmoja ambaye anaendesha vyombo vya usafiri, ajitafakari namna anavyoweza kukiendesha chombo chake.
ajali nyingi za barabarani zinaonyesha kuwa zinasababishwa na mwendo kasi wa madereva, au kujaza abiria na mizigo kupita kiasi.
Video Mpya : KAMBI YA NYANI Ft. JULIESO - KICHWA
6 hours ago
No comments:
Post a Comment